Please Wait
12076
- Shiriki
Neno Tharu-Llahi (ثار الله) limekuja likiwa na maana mbili: moja ni kwa maana ya damu, na ya pili ni kwa maana ya kulipiza kisasi na kutaka kummwga damu ya muuwaji.
Kwa hiyo maana ya mwanzo inapotumika kwa ajili ya kumuita Yeye (a.s) Tharu-Llahi (ثار الله), huleta maana ya kuwa: Mola weke Ndiye pekee awezaye kudhamini kisasi cha mauwaji Yake (a.s), na pia Mola Ndiye mhusika hasa anayewasimamia na kuwatetea wale wote wenye kuuza roho zao kwa ajili ya Mola wao.
Lakini pia Yeye (a.s) huitwa Tharu-Llahi (ثار الله), huku ikikusudiwa maana ya pili ya neno hilo, huku neno (ثار الله), likiwa na maana ya (damu ya Mungu), kinachokusudiwa katika kumuita Yeye (a.s) jina hilo ni moja ya maana zifuatazo:
- Kuitukuza damu ya Imamu Husein (a.s) kwa kutokana na kuwa Yeye (a.s) alikubali damu yake imwagwe kwa nia ya kuinusuru dini ya Mola wake.
- Mtu anapofikia daraja kuu ya ucha-Mungu, huwa anaangalia kwa jicho la Mola wake na anachukua na kushika anachokishika kwa mkono wa Mola wake, pia ulimi wake hugeuka kuwa ndiyo spika ilioko mbele ya jukwaa la Mola wake, hivyo basi yeye huwa ndiye uwanja wa kudhihiri matokeo mbali mbali ambayo Mola hutaka kuyaleta katika ulimwengu huu, na mtu kama huyo huwa siku zote yuko tayari kuunywesha mti wa Uislamu damu yake iliyo safi yenye uhai, huku akiwa na imani ya kuwa damu hiyo ni ya Mola Mtukufu na ni lazima itumike kwa ajili ya kumtumikia Mola huyo katika hali zote, iwe ni katika ule wakatia ambao damu hiyo imo ndani ya mwili wake, au pia pale inapohitajika damu hiyo kumwagika kwa ajili ya kumstiri mja mpenzi wa Mola au dini ya Mola.
Maana ya pili miongoni mwa maana hizo, ni maana bora zaidi iliyobeba uhakika kamili wa tokeo zima la Karbala, huku ikidhihirisha uhakika kamili wa Johari ya Imamu Huseni (a.s), hii ni kwa kila mwenye kutaka kuufahamu ukweli na haki.
Kuhusiana na uhakika wa jina hili, ni kwamba jina hili limetumika kwa kuwaita Maimamu wawili, nao ni Imamu Ali na Imamu Husein (a.s). Pale sisi tunapotoa salamu zetu za heshima kwa Imamu Husein (a.s), huwa tunasema hivi:
«السَّلَامُ عَلَيْكَ يَا ثَارَ اللَّهِ وَ ابْنَ ثَارِهِ»؛
Maana yake ni kwamba: “Amani iwe juu yako ewe damu ya Mola na mwana wa damu ya Mola”.[1]
Kuhusiana na maana ya neno (damu ya Mola) sisi tunaweza kulitumia neno hili katika moja kati ya maana zifuatazo:
- Mlipizaji kisasi: iwapo tutalifasiri neno hilo katika maana hii, hapo kilichokusudiwa kitakuwa ni kuwa, Mola ndiye pekee Ambaye anaweza kulipiza kisasi ipaswavyo kwa yule aliyemdhulumu walii wake (iwe ni Imamu Husein au Imamu Ali (a.s).
Pia ni muhimu kuelewa kuwa lile kundi lililoamua kufanya maandamano dhidi ya utawala wa Yazid, huku likiwa katika njia ya kutubia kwa kule kumuacha mkono Husein (a.s), lilitumia tamko:
«یا لثارات الحسین»
Walilitumi tamko hilo kwa ajili kumaanisha kuwa: wao wamesimama kwa ajili ya kulipiza kisasi cha Imamu Husein (a.s), pia Mukhtari naye aliutumia usemi huo katika mapinduzi yake yaliyoleta mageuzi ndani ya utawala wa Yazid, na mwishowe kuuangusha utawala huo.[2] Vile vile « یا لثارات الحسین» ndio utajo wa Malaika waliokaa juu ya kaburi la Imamu Husein (a.s), ambao wapo juu ya kaburi hilo hadi atakapodhihiri Imamu Mahdi (a.f),[3] pia huo ndio utakataokuwa utajo na ulingano wa Imamu Mahdi (a.s) pale ataposimama na kuitetea haki, na huo ndio ulingano wa wafuasi wake.[4]
Maana ya neno «ثارالله» ambayo tumeifafanua hapo juu, ndiyo iliyokubalika mbele ya wanachuoni wengi wa Kiislamu,[5] hapa basi neo «ثارالله» litakuwa na maana ya mtu ambaye thamani ya damu yake iko kwenye mkono wa Mola Mtukufu, Naye ndiye atakayemrejeshea thamani hiyo, kwani Imamu Husein (a.s) hakupoteza maisha yake kwa ajili ya familia yake, kiasi ya kwamba iambiwe kuwa familia yake ndiyo yenye jukumu la kulipiza kisasi na kumlipa yeye thamani ya damu yake. Imamu husein (a.s) ni mtu aliyefungamana na kila muungwana Naye (a.s) ni kiongo muhimu cha ulimwengu wa kimaana, na fungamano lake hasa liko kwenye Dhati Takatifu ya Mola wake, kwa hiyo mlipizaji bora wa kisasi ni Mola Mwenyewe (s.w), na kisasi cha baba yake pia ambaye ameiuza nafsi yake kwa Mola wake, kitachukuliwa na Mola Mtakatifu.
2 – Na wakati mwengine neno hili huwa na maana ya (damu ya Mwenyezi Mungu), kinachofahamika kutoka kwa mwanachuoni maarufu Majlisiy kuhusina na neno «ثارالله» ni kuwa neno hili lina maana ya (damu au mtakaji damu ambaye hujulikana kuwa ni mtaka kisasi);[6] pia chenye kutilia mkazo maneno yake, ni yale maelezo ya kamusi ya (Lisanul-arab) kuhusiana na maana ya neno «الثار». Kamusi ya (Lisanul-arab) kuhusiana na neno hilo inasema: “maana ya neno (الثَّأْرُ) ni kule mtu kutaka kisasi, au pia imesemwa kuwa, neno hili lina maana ya damu”.[7]
Lakini je kuiita damu ya Imamu Husein (a.s) kuwa ni damu ya Mungu!, huwa ni sawa?
Jawabu ya swala hili ni kwamba: kuna aina mbali mbali za maneno ambayo yanaonekana kutumiwa ndani ya tamaduni za Kiislamu, na baadhi ya maneno hayo ni kama vile: neno (mkono wa Mungu), lakini maneno haya huwa hayamaanishi kuwa Mungu ni mwenye kiwiliwili, bali huwa kuna maana maalumu inayokusudiwa huku likitumika neno hilo kuwa ni kama nyenzo maalumu yenye kuleta rangi maalumu kwa ajili ya kuipamba na kuiboresha maana kamili inayokusudiwa kupitia neno hilo, ili maana hiyo ieleweke vyema zaidi;[8] kwa mfano pale isemwapo kuwa Ali (a.s) ni mkono wa Mungu, huwa haikusudiwi kuwa Mungu ana kiwiliwili kama vile mwanaadamu, kisha mkono wake ndio huyo Ali (a.s), bali makusudio ya usemi huo, ni kwamba Ali (a.s) ni moja kati ya dalili za nguvu za Mola Matakatifu.
Hivyo basi sisi tunaweza kumuita Imamu Husein (a.s) kuwa ni «ثارالله» (damu ya Mungu) kupitia moja kati ya sababu zifuatazo:
1- tunaiegemeza damu Yake (a.s) kwa Mungu kwa kutaka kumpa utukufu maalumu, kwa kutokana na kuwa damu hiyo imemwagwa kwa ajili ya kuitetea dini ya Mola Mtukufu, kama vile alivyotukuzwa ngamia aliyechinjwa na wabishi waliotajwa katika Qur-ani, ngamia ambaye alitukuzwa kwa kuliitwa kuwa ni ngamia wa Mungu «هذِهِ ناقَةُ اللَّه».[9]
Pia kuna Aya mbali mbali za Qur-ani zenye kuvihusisha baadhi ya vitu na Mola Mtukufu, na baadhi ya vitu hivyo ni kama vile «بیت الله» (nyumba ya Mungu), hapa nyumba imeegemezwa kwa Mungu kwa ajili ya kuipa nyumba hiyo (Kaaba) utakaso na umuhimu maalumu.[10]
2- Mja aliyekamilika kiimani na kiucha-Mungu pale anapobobea kiimani, hugeuka kuwa yeye ni mkono na ulimi wa Mola wake, na huwa yuko tayari kuimwaga damu yake kwa ajili ya dini ya yake, hapo basi Mola humtumia mja wake huyo kwa kupitia ulimi wake, mkono wake na nguvu zake kwa ajili ya maslahi mbali mbali ya waja wake, pia damu ya mtu huyo huwa iko tayari kwa ajili ya kuihudumia dini ya Mola wake, hivyo basi pale inapojiri yeye kukabiliana na wakorofi kiasi ya kwamba damu yake itakuwa hatarini, yeye huwa yuko tayari kwa hilo, kwani yeye hakioni chochote kila alichokuwa nacho kua ni milki yake. Imamu Husein pamoja na baba yake Ali (a.s) walikuwa katika daraja za juu kabisa za ucha-Mungu, jambo ambalo liliwafanya wao kutothamini chochote kile zaidi ya Mola wao. Kwa vyovyote vile ambavyo mtu atona, lakini lililokweli ni kuwa lakabu ya «ثارالله» ni lakabu maalumu mbayo inaonekana kwenye vitabu kutumika kwa ajili ya Imamu Husein (a.s). Sisi tunaamini kuwa maana ya pili ya neno hili ndiyo maana bora zaidi, ingawaje kuitumia maana ya kwanza ya neno hilo huwa si tatizo. Kwa kutokana na kuwa Yeye (a.s) aliitumia damu yake kwa ajili ya kuupa uhai Uislamu, ndiyo maana ikasemwa kuwa: “Uislamu umekuja kupitia Muhammad (s.a.w.w), na umedumu kupitia Husein (a.s).
[1] Rejea kitabu (Alkaafi) cha Muhammad bin Yaaquub Koleiniy, juz/4, uk/576.
[2] Rejea kitabu (Bihaarul-anwaar) cha Muhamaad Baaqir Majlisiy, juz/45, uk/333.
[3] Imeelezwa kuwa: Malaika 4000 walishuka kwa ajili ya kumpa msaada Imamu Husein (a.s), lakini walipofika Karbala, walimkuta (a.s) tayari ameshauwawa, Malaika hao hadi leo wapo juu ya kaburi Lake (a.s), huku wakiwa wanyonge waliojawa na vumbi, na watabakia katika hali hiyo hadi atakapodhihiri Imamu Mahdi (a.s), ambapo wao watashikamana Naye huku wakisema : «يا لثارات الحسين». Rejea kitabu (Aamaal) cha sheikh Saduuq, uk/130, almajlis- saabi’u wa ishruun. Rejea (Bihaarulanwaar) cha Muhammad Baaqir Majlisiy, juz/44, uk/286.
[4] Rejea kitabu (Muntahal-aamal) cha sheikh Abbaasi Qummiy, juz/ uk/542, pia kitabu (Bihaarul-anwaar), juz/44, uk/218, pia kitabu (Bihaarul-anwaar), juz52, uk/308.
[5] Muandishi wa tafsiri ya Qur-ani (Tafsiri nemune), anasema: neno (thaaru) halijaonaekana hata mara moja ndani ya Qur-ani likiwa na maana ya damu, bali limekuja likiwa na maana ya (thamani ya damu), ama neno hilo katika lugha ya Kiarabu huwa lina maana ya (damu); Rejea kitabu (Tafsiri nemune), juz/4, uk/229.
[6] Yeye alipokuwa akiifasiri ibara isemayo: «و أنك ثار الله في الأرض» alisema: “maneno haya yana maana ya kuwa Imamu Husein (a.s), ni mtu ambaye amemtafuta Mola wake kwa kupitia damu yake, yaani amemwaga damu yake kupitia adui zake kwa ajili ya kufika kwa Mola wake, pia ina maana ya kuwa Yeye (a.s) ndiye atakayesimama kidete katika siku ya marejeo kwa ajili ya kutaka kulipiza kisasi juu ya damu Yake (a.s) pamoja na damu ya Ahlu-Baiyt (a.s) kwa amri ya Mola wake. Rejea kitabu (Bihaarul-anwaar) cha Muhammad Baaqir Al-Majlisiy, juz/98, uk/151.
[7] Rejea kamusi (Lisanul-arab) la Ibnu Mandhuur, juz/4, uk/97.
[8] Angalfia tafsiri Nemune ya Naasir Shirazi, juz/4, uk229, pia tafsiri Nuur ya Muhsin Qiraatiy, juz/2, uk/443.
[9] Suratu Huud Aya ya 64.
[10] Rejea kitabu (Taqriibul-Qur-ani ilal-adh-haani) cha Sayyid Muhammad Huseiniy Ahirazi, juz/2, uk/200.